//
you're reading...
Uncategorized

Maswali 10 Muhimu Kuhusu FATIMA Sasa YANAJIBIWA!

MUUJIZA WA FATIMA
1. Ujumbe wa Fatima ni Nini?

Ujumbe wa Fatima ni idadi kadhaa ya utabiri, maagizo, maonyo na ahadi, kuhusu Imani na dunia ambavyo vililetwa kwetu na Bikira Maria Mbarikiwa kwa watoto watatu wachungaji — Lusia, Yasinta na Fransisi — kwa njia ya matukio yaliyofuatana huko Fatima, Ureno kuanzia Mei hadi Oktoba 1917.

2. Kwa Nini ni Lazima Niuamini Ujumbe wa Fatima?

Ni lazima uuamini Ujumbe wa Fatima kwa sababu:

(1) Ulithibitishwa na muujiza wa wazi usio na kifani, Muujiza wa Jua, uliotokea kwa muda ule ule ambao Lusia alisema ungetokea. Zaidi ya watu 70,000, wakiwemo Wapagani, Wakomunisti na watu wasiomuamini Mungu, waliliona jua, kinyume na kanuni zote zinazohusu ulimwengu mzima, likizunguka upesi angani, likitupa nuru yenye rangi mbalimbali na kushuka duniani. Tukio hili liliandikwa katika magazeti sehemu mbalimbali za dunia, likiwemo gazeti la New York Times.

(2) Baba Watakatifu wote tangu Muujiza wa Fatima utokee wamekiri kwamba Ujumbe huo ni wa kweli. Baba Watakatifu kadhaa wamewahi kwenda Fatima wao wenyewe, wakiwemo Paulo VI, Yohani Paulo I na Yohani Paulo II. Yohani Paulo II alisema huko Fatima mwaka 1982 kwamba “Ujumbe wa Fatima unaamuru jambo linalobidi kufuatwa na Kanisa.”

(3) Miujiza mingine mingi imewahi kufanywa na Mungu ikithibitisha kwamba Ujumbe wa Fatima unatoka Kwake, sio tu wakati wa Muujiza wa Jua, wa tarehe 13 Oktoba 1917, lakini kwa miaka mingi hadi hivi leo, miujiza ya wongofu na kuponywa magonjwa ambayo sayansi haiwezi kuelezea kwa njia za asili.

(4) Ujumbe wa Fatima ulitabiri kwa usahihi matukio ya dunia, kitu ambacho kinathibitisha kwamba ni utabiri wa kweli.

3. Ujumbe wa Fatima Ulitabiri Nini?

Ujumbe wa Fatima ulitabiri kwa usahihi mwaka 1917 matukio yote yafuatayo, ambayo yalitokea:

(1) Mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia;

(2) Kuibuka kwa Urusi kama nchi yenye nguvu duniani ambayo “ingesambaza makosa yake (ukiwemo Ukomunisti) duniani kote…na kuzusha vita na maangamizi dhidi ya Kanisa”;

(3) Kuchaguliwa kwa Baba Mtakatifu atakayeitwa Pius XI;

(4) Kutokea kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kufuatia mwanga wa ajabu angani wakati wa usiku.

Ujumbe wa Fatima pia ulitabiri kwamba kama maagizo ya Bikira Maria huko Fatima hayakutimizwa, roho nyingi zitapotea, “Baba Mtakatifu atapata mateso mengi”, kutaendelea kuwa na vita na maangamizi ya Kanisa na “mataifa mbalimbali yataangamizwa.” Kuangamizwa kwa mataifa kulikotabiriwa huko Fatima bado hakujatokea, lakini wengi wanahofu kwamba kutatokea hivi karibuni, kutokana na kuongezeka kwa uovu na rushwa duniani.

4. Ujumbe wa Fatima Unaagiza Nini?

Huko Fatima Mama Yetu alisema kwamba Mungu alitaka kuanzisha duniani ibada kwa Moyo Safi Kabisa wa Maria. Mama Yetu alisema kwamba roho nyingi zingeokolewa kutoka Jehanamu na maangamizi ya mataifa yangezuiliwa, iwapo, katika muda unaofaa, ibada kwa Moyo Wake Safi Kabisa ingeanzishwa hasa kwa njia hizi mbili:

(1)Baba Mtakatifu pamoja na maaskofu Wakatoliki wa dunia nzima kuitolea nchi ya Urusi kwa Moyo Safi Kabisa wa Maria kwa ibada ya wazi ya kidini, na

(2) Ibada ya kila Jumamosi ya kwanza kwa miezi mitano mfululizo ya kupokea Komunyo Takatifu (na ibada maalum nyingine za muda wa nusu saa) kwa malipizi ya dhambi zilizotendwa dhidi ya Bikira Maria Mbarikiwa — utaratibu unaojulikana kwa Wakatoliki kama “ibada ya Jumamosi ya Kwanza”.

5. Je, Maagizo Haya ya Mama Yetu wa Fatima Yamekwishatimizwa?

Hapana, sio yote inavyotakiwa. Baadhi ya Waumini wanafanya ibada ya “Jumamosi ya Kwanza”, lakini Urusi bado inahitaji kutolewa kwa Moyo Safi Kabisa wa Maria kwa ibada ya wazi ya kidini ikiongozwa na Baba Mtakatifu pamoja na maaskofu Wakatoliki wa dunia nzima.

Mnamo mwaka 1982 mtokewa wa mwisho ambaye yungali hai,Sista Lusia, ambaye hivi sasa ni mtawa aliyejitenga kwa ajili ya dini anayeishi Coimbra, hukoUreno, aliulizwa iwapo kutolewa kwa Urusi kulikofanywa na Baba Mtakatifu Yohani Paulo II kulikuwa kumetosheleza. Alijibu kwamba hakukutosheleza, kwa sababu Urusi haikutajwa, na maaskofu wa dunia nzima hawakushirikishwa. Kutolewa kwingine kwa Urusi mwaka 1984 vile vile hakukuitaja Urusi au kuwajumuisha wengi wa maaskofu wa dunia, na Sista Lusia alisema mara tu baadaye, kwamba kutolewa huku kulikuwa kumeshindwa kutimiza maagizo ya Mama Yetu.

6. Ujumbe wa Fatima Unaonya Nini?

Unaonya kwamba iwapo maagizo ya Mama Yetu juu ya kuitolea Urusi na ibada ya Jumamosi ya Kwanza havitatimizwa, Kanisa litaangamizwa, kutakuwa na vita kubwa nyingine, Baba Mtakatifu atapata mateso mengi, na mataifa mbalimbali yataangamizwa. Mataifa mengi yatakuwa chini ya utumwa wa wapiganaji wa Kirusi wasiomuamini Mungu. Zaidi ya yote, roho nyingi zitapotea.

7. Ujumbe wa Fatima Unaahidi Nini?

Ujumbe wa Fatima unaahidi kwamba kama maagizo ya Mama Yetu wa Fatima yatatimizwa “Moyo Wangu Safi Kabisa utashinda. Baba Mtakatifu ataitolea Urusi Kwangu, ambapo Urusi itaongoka wanadamu watajaliwa na kipindi cha amani.

8.Je, Sio Kweli Kwamba Kutolewa kwa Urusi Kulifanyika mwaka 1984 na Kwamba “Kuanguka kwa Ukomunisti” Kunathibitisha Kuwa Kutolewa Huko Kulitimiza Lililokusudiwa na Kwamba Urusi Hivi Sasa Inaongoka?

Hapana, sio kweli. Tunajua kuwa sio kweli kwa sababu:

(1) Tarehe 25 Machi 1984, baada ya kuitolea dunia, Baba Mtakatifu Yohani Paulo II alisema mara mbili kwamba agizo la Mama Yetu wa Fatima juu ya kuitolea Urusi halikuwa limetekelezwa.

(2) Mara baada ya kutolewa huko kulikofanywa 1984, ambako hakukuitaja Urusi wala kuhusisha kushiriki kwa maaskofu wote Wakatoliki wa dunia, Sista Lusia alisema kuwa hakutoshelezi kwa sababu hakukufuata maagizo yaliyotolewa kwake na Mama Yetu.

(3) Tangu 1984 hali ya dunia ya kimaadili na kiroho ni wazi imeharibika mno: Katika miaka 14 iliyopita kumekuwa na matukio milioni 600 ya utoaji mimba, na vita vimelipuka duniani kote. Uuaji kwa kuwahurumia wagonjwa ambao wanaugua maradhi yasiyoponyeka na matendo ya kujamiiana kinyume na maumbile “vimeidhinishwa kisheria”. Katika nchi ya Urusi yenyewe sheria mpya imepitishwa ambayo inalikandamiza Kanisa Katoliki na kutoa upendeleo kwa dini ya Kiislamu, Buddha, Wayahudi na makanisa ya Kiothodoksi ambayo yalivamia parokia za Kikatoliki chini ya Wakomunisti. Hivyo, ni wazi kwamba Urusi haijaongoka kwa imani ya Kikatoliki kama jinsi Mama Yetu wa Fatima alivyoahidi ingetokea iwapo agizo lake lingetimizwa.

(4) Kumekuwa na wongofu wa watu wachache sana kuingia Ukatoliki nchini Urusi katika muda wa miaka kumi na minne iliyopita. Katika nchi nzima ya Urusi leo hii kuna Wakatoliki 300,000 tu – idadi ambayo ni chini kabisa ya asilimia moja ya watu wote wa nchi ya Urusi. Kwa kulinganisha, baada ya Mama Yetu kutokea huko Guadalupe, nchini Mexico mnamo karne ya 16, zaidi ya watu milioni 7 wa Mexico, waliongoka kutoka katika upagani na kufuata imani ya Kikatoliki katika muda wa miaka tisa na Mexico ikawa nchi ya Kikatoliki.

9. Je, Kwa Nini Ujumbe wa Fatima ni Muhimu Kwangu na Familia Yangu?

Ujumbe wa Fatima ni muhimu kwako na familia yako kwa sababu inahusu wokovu wa roho, amani duniani na, kama maagizo ya Mama Yetu hayatatimizwa, matokeo yake ni kuangamizwa kwa mataifa na kuwa chini ya utumwa wa wapiganaji wa Kirusi wasiomuamini Mungu.

10. Je Lakini, Ujumbe wa Fatima Sio Ufunuo wa Binafsi Tu Ambao Mkatoliki Hahitaji Kuuamini?

Hapana, sio tu ufunuo wa binafsi. Ni ufunuo wa wote, wa kinabii uliotolewa na Bikira Maria, Mama wa Mungu. Usichanganywe na “Ufunuo” au kama unavyoitwa pia, Amana ya Imani, iliyomalizika na kifo cha Mtume wa mwisho. Lakini ufunuo wa wote wa kinabii hautakiwi kudharauliwa. Utabiri wa Bikira Maria ulithibitishwa na muujiza wa wazi na kuthibitishwa kuwa ni wa kweli na idadi kubwa ya Baba Watakatifu. Pia, utabiri wake umetokea.

Kwa hiyo, wakati kuamini katika Ujumbe wa Fatima huenda kusihitajike kabisa kwa Wakatoliki kama sharti la imani, mtu atakuwa mjinga sana kuupuuza ujumbe huu wa kweli na wa wazi kutoka Mbinguni. Kama Mt. Paulo alivyofundisha: “Msidharau utabiri, lakini thibitisheni vitu vyote; zingatieni kile ambacho ni kizuri.” (1 Wath. 5:20-21) Utabiri wa Fatima umethibitishwa kwa kiasi ambacho unastahili kuaminiwa. Hatutakiwi kuudharau, badala yake tuzingatie katika yale aliyotuambia Mama Yetu pale Fatima.

Discussion

No comments yet.

Leave a comment

Recent Comments

Archives

Categories